Wednesday, September 20, 2017

Tetemeko laua zaidi ya watu 200 Mexico

Tetemeko baya la ardhi limekumba maeneo ya katikati mwa Mexico na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 200.
Tetemeko lenye nguvu ya kipimo cha saba nukta moja limedondosha karibu majengo 30 katika mji mkuu wa Mexico city.
Watu wanaotoa huduma za dharura wakisaidiwa na mamia ya watu wanaojitolea bado wanaendelea kutafuta manusura ambao wamefukiwa na kifusi.

Maafisa wa serikali nchini wanasema idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka.
Daniel Lieberson alikuwa katika hotel ya Hilton Mexico City wakati tukio hilo likitokea.
''...Nilikuwa katika ghorofa ya 26. jengo lilikuwa likiyumba mbele na nyuma vioo vyote vilivunjika na tuliogopa kwamba madirisha yatavunjika, lakini haikuwa hivyo. Lakini mashine ya kutengenezea kahawa na vitu vingine vilianguka chini vyote, meza, ilikuwa shida kweli, lilidumu kwa sekunde thelathini tu, lakini ilionekana kama limedumu daima...'' anasema Daniel Lieberson
Kwa upande wake Natasha Pizzey mwandishi wa habari katika mji huo anasema kuna idadi kubwa ya watu waliofukiwa na kifusi baada ya majengo kuporomoka..Tunafahamu kuna watu walionusurika katika majengo ya makazi yaliyoporomoka, hatukuwa na uwezo wa kuwaokoa. Kuna mamia ya wafanyakazi wa kujitolea waliokwenda katika eneo la tukio...'' ameongezea kusema
Aidha pia kumetokea madhara mabaya katika majimbo ya jirani ya Morelos na Puebla.
Mapema mwezi huu tetemeko hilo la ardhi pia lilipita katika eneo la pani ya kusini magharibi mwa Mexico na kusababisha vifo vya watu 90..


Leicester City wawatupa nje Liverpool Kombe la Carabao

Islam Slimani alifunga bao kwa kombora kali na kuwasaidia Leicester kuwalaza Liverpool 2-0 katika mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la Carabao, ambao pia hufahamika kama Kombe la EFL, uwanjani King Power Jumanne.
Mchezaji huyo wa Algeria alifunga kwa mguu wa kushoto baada ya nguvu mpya Shinji Okazaki kuwaweka Leicester kifua mbele.
Mabao hayo yalipatikana baada ya Liverpool kutawala kipindi cha kwanza ambapo Philippe Coutinho alikuwa amecheza vyema sana kabla ya kuondolewa uwanjani.
Okazaki aliingia uwanjani na kuwaongezea nguvu Leicester na kufunga kutoka kwa pasi safi iliyotoka kwa Vicente Iborra.
Alex Oxlade-Chamberlain na Dominic Solanke walionunuliwa na Liverpool majuzi wote walipoteza nafasi nzuri za kufunga.
Kwingineko Roy Hodgson alipata ushindi wake wa kwanza Crystal Palace wakiwa nyumbani dhidi ya Huddersfield.
Bristol City nao waliwashangaza Stoke City.
Tottenham nao walichukua dakika 65 kuwapangua Barnsley uwanjani Wembley nao Leeds wakawalaza Burnley kwa mikwaju ya penalti uwanjani Turf Moor.
Liverpool watasafiri tena Leicester kwa mechi ya Ligi ya Premia siku ya Jumamosi, mechi ambayo itaanza saa moja unusu jioni saa za Afrika Mashariki.chanzo bbc swahili

Haye ataka kukipiga kwa mara nyingine na Bellew

Bondia David Haye amesema yupo tiyari kurudia mpambano na Tony Bellew.
Mpambano wao wa raundi 11 uliishia raundi ya 6 walipokutana mwezi Machi.
Haye alipigwa ndani ya raundi ya sita kwa makonde ya mfululizo yaliyompeleka chini.
Ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba'' imechukua miezi kadhaa ya majadiliano na sasa ni muda wa kwenda tena ulingoni.

Hakuna tarehe wala sehemu kamili mpambano huo utakapofanyika, lakini baadhi ya taarifa zinasema utafanyika Disemba 17, kwenye uwanja wa London O2.
Haye alifanyiwa upasuaji baada ya kuchapwa vibaya na Bellew mzaliwa wa Liverpool na tokea kupona kwake amekuwa akifanya mazoezi na walimu wake Shane McGuigan

Monday, September 18, 2017

Serikali ya Tanzania yaendelea kuzuia almasi ya kampuni ya Petra

Shughuli zimeanza tena katika mgodi mkubwa zaidi wa madini ya almasi nchini Tanzania, licha ya mzozo na serikali ya Tanzania, ambayo ilikamata bahasha iliyokuwa na almasi kwenye uwanja wa ndege.

Shughuli katika mgodi wa Williamson zimerejeshwa baada ya kusimamishwa kwa siku nne.
Wiki moja iliyopita hisa kwenye kampuni ya Uingereza ya Petra zilishuka kwa asilimia 7, baada ya almasi zake kuzuiwa kusafirishwa kutoka nchi Tanzania, ambapo pia wafanyakazi wake kadha walihojiwa na mamlaka za nchi hiyo.
Mamlaka zilikamata bahasha iliyokuwa na almasi ambayo hadi sasa haijaachiliwa.
Mazungumzo ya kampuni na serikali kuhusu suala hilo yanaendelea, kwa kujibu wa kampuni ya Petra.
Kampuni hiyo kubwa zaidi ya kuchimba almasi nchi Tanzania inalaumiwa kwa kuzusha thamani ya almasi zake.
Serikali inasema kuwa Petro iliandika mzigo huo kuwa wa thamani ya dola milioni 14.6 wakati thahamia yake halisi ilikuwa dola milioni 29.5.
Petro ilikana madai hayo, ikisema kuwa serikali ndiyo inahusika kwa kuthibitisha thamani kama hiyo.
Mgodi wa Williamson ulio kaskazini magharibi mwa Tanzania unamilikiwa na Perto kwa asilimia 25 huku serikali ya Tanzania ikimiliki asilimia 25.chanzo na bbc swahili

Fury aomba hukumu ya kufungiwa ndondi kuondolewa

Bondia wa zamani wa uzito wa juu duniani Tyson Fury ameomba kuondolewa adhabu ya kutoshiriki mchezo huo ikiwa ni karibia mwaka mzima tokea kufungiwa.
Fury mwenye miaka 29, hajapigana tokea alipomtwanga Wladimir Klitschko Novemba 2015.
Mahakama ilisogeza mbele kusikilizwa kwa kesi yake na mpaka sasa bado haijapangwa tena.
''Ni kwa muda gani nitakaa nje ya ulingo?'' Fury aliandika kwenye mtandao wa Twitter.
''Safisheni jina langu na mniache nirejee kufanya kile ninachokipenda.Sina kosa, niachieni huru!''
Fury atapaswa kuhojiwa na bodi ya kuzuia matumizi ya dawa zilizokataliwa michezoni na baada ya hapo watatoa uamuzi.chanzo na bbc swahili

Rooney ahukumiwa kutoendesha gari kwa miaka miwili

Nahodha wa zamani watimu ya taifa ya England Wayne Rooney amehukumiwa kutoendesha gari kwa miaka miwili sambamba na kufanya kazi za jamii kwa saa 100.



Rooney 31, alikamatwa kwenye kitongoji cha Wilmslow, Cheshire kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa Rooney pia atalipa faini ya Pauni 170 kwa kosa hilo.
''Nimekubali kosa langu na nimeomba radhi kwa familia, klabu yangu ya Everton, mwalimu na sasa ni zamu ya mashabiki.Ninaomba radhi kwa kitendo kile.'' alisema Rooney baba wa watoto watatu. 1.
Mchezaji huyo aliyezaliwa katika jiji la Liverpool alijiunga na Everton klabu yake ya utotoni akitokea Manchester United miaka 13 baada ya kuondoka.chanzo bbc swahili

KOCHA NJOMBE MJI ANG’ATUKA BAADA YA KUPIGWA MECHI TATU MFULULIZO

TIMU ya Njombe Mji imepata pigo baada ya kocha wake Mkuu, Hassan Banyai kung’atuka kufuatia matokeo mabaya katika mechi tatu za mwanzo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 
Njombe Mji FC imefungwa mechi zote tatu za mwanzo za Ligi Kuu, mbili nyumbani Uwanja wa Saba Saba dhidi ya Tanzania Prisons 2-0 na Yanga SC 1-0 kabla ya kuchapwa 1-0 na Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Na kabla ya kuingia kwenye mchezo wa nne dhidi ya Ruvu Shooting Septemba 23, mwaka huu, leo Njombe Mji imetoa taarifa ya kutengana na kocha wake aliyeipandisha timu Ligi Kuu msimu huu.
Afisa Habari wa Njombe Mji FC, Solanus Mhagama amesema kwamba kwa kipindi hiki, aliyekuwa Kocha Msaidizi, Mrage Kabange ndiye ataiongoza timu hadi hapo uongozi utakapotoa tamko longine.
Njombe Mji imemshukuru Banyai kwa mchango wake kwenye timu ikiwemo kuipandisha Ligi Kuu na kumtakia kila la heri huko aendako.
Mhagama amesema kwa sasa wanaelekeza nguvu kwenye mchezo wao ujao dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani mwishoi mwa wiki.