Tuesday, September 27, 2016
Wednesday, September 21, 2016
Taarifa ya polisi kuhusu ajali ya basi la Super Shem Mwanza
September 21, 2016 imetokea ajali ya barabarani jijini Mwanza ambayo imehusisha mabasi mawili likiwemo basi la Super Shem lenye namba za usajili T 874 CWE ambalo lilikuwa likitokea Mbeya limegongana na Basi dogo aina ya Hiace yenye namba za usajiliT 368 CWQ iliyokuwa inatokea kijiji cha Shirima na kusababisha vifo vya watu 11 na majeruhi kadhaa.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi ambapo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza chanzo cha ajali kuwa ni Hiace iliyogongwa na basi la Super Shem kuingia barabara kuu bila kufuata sheria. Ajali hiyo imetokea eneo la Mwamaya Makutano Kwimba.
>>>Kati ya waliofariki, wawili ni watoto wadogo, majeruhi saba huku miili ya marehemu na majeruhi wakikimbizwa Hospitali ya Ngudu, Dereva wa Super Shem alipata madhara, lakini wengi zaidi waliopata madhara ni kutoka kwenye Hiace ndiko kuna matatizo makubwa:- Kamanda Ahmed Msangi
Tuesday, September 20, 2016
Perez, Xhaka watakata na kuipa ushindi mnono Arsenal EFL Cup
Mshambuliaji mpya wa Arsenal aliyesajili kutoka Deportivo La Coruna Lucas Perez leo amefungua ukurasa wa ambao kwa kufunga magoli mawili kwenye ushindai wa 4-0 kwa Arsenal kwenye mchezo wa Kombe la EFL dhidi ya Nottingham Forest inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza na kufanikiwa kufuzu raundi ya nne
Granit Xhaka alikuwa wa kwanza kufunga goli baada ya kupiga shuti kali kutoka umbali wa mita 30 na kuipa Arsenal goli la kuongoza.
Mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Nicklas Bendtner almanusura afunge bao lakini shuti lake lilitoka nje.
Baadaye Lucas Perez aliifungia Arsenal bao la pili kwa penati baada ya Chuba Akpom kufanyiwa madhambi kwenye eneo la hatari.
Lucas kwa mara nyingine tena alifunga bao tatu na la pili kwa upande wake kabla ya Alex Oxlade-Chamberlain kuhitimisha karamu ya ushindi kwa kufunga bao la nne mnamo dakika ya 90.
Aliyeng’atwa ulimi Singida mbaroni

ZIKIWA zimepita siku saba tangu kijana Saidi Mnyambi (26) ang’atwe ulimi na jirani yake, Mwajabu Jumanne (36) hadi kupoteza uwezo wa kuongea na kula, hatimaye Jeshi la Polisi limesema linawashikilia wote wawili kwa uchunguzi zaidi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Peter Kakamba alisema mjini hapa jana kuwa polisi imelazimika kuwashikilia wote wawili kutokana na maelezo yao kutofautiana.
Alisema wakati kijana huyo anadai kuwa tukio hilo lilitokea baada ya yeye kulazimishwa kufanya mapenzi, mwanamke huyo naye anadai kuwa alimng’ata ulimi wakati akijaribu kujiokoa ili asibakwe.
Kutokana na hali hiyo, Kamanda Kakamba alisema jeshi hilo limeona kuna haja ya kuwashikilia wote wawili kwa uchunguzi zaidi ili kubaini ukweli wa jambo hilo kabla ya kuwafikisha mbele ya Mahakama.
Mnyambi alinyofolewa theluthi moja ya ulimi wake na mke wa jirani yake kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kumlazimisha kufanya naye mapenzi Sikukuu ya Idd El Hajj saa 3.30 usiku.
Alidai kuwa siku ya tukio, mwanamke huyo alimwomba amsindikize nyumbani kwake kwa kuwa alikuwa amelewa.
Hata hivyo, walipofika njiani inadaiwa kuwa mama huyo alimtaka kijana huyo wafanye mapenzi jambo ambalo alimkatalia lakini akamwomba waagane, angalau kwa kunyonyana ulimi (ampe denda), lakini ghafla kijana huyo alishtukia aking’atwa ulimi na mama huyo na kukimbilia nyumbani kwake.
Muuguzi Mwandamizi Hospitali ya Mkoa wa Singida alikolazwa kijana huyo, Herman Mallya amesema kuwa hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri ingawa hajapata uwezo wa kuongea.
Alichozungumza Obama kwenye hotuba yake ya mwisho mkutano wa UN

Mkutano wa mkuu wa Umoja wa Mataifa, United Nations General Assembly (UNGA) umeanza wiki hii nchi Marekani katika jiji la New York, na kushuhudiwa viongozi wa mataifa mbalimbali wakihutubia mkutano huo utakaojadili masuala makubwa yanayoikabili dunia kwasasa ikiwemo suala la wakimbizi, utawala wa haki na demokrasia, uchumi na mengineyo.
Kupitia hotuba aliyoitoa Rais wa Marekani Barack Obama ameyataka mataifa tajiri kufanya kila linalowezekana kuwasaidia watu wanaokimbia vita huku akikiri kuwa dunia inakabiliwa na changamoto nyingi na kuzitaka nchi tajiri kuchukulia tatizo hilo kama ni lao huku akisema kuwa ongezeko la wakimbizi ni ishara ya vita na mateso na kwamba hali hiyo itaweza kushughulikiwa tu endapo migogoro kama ule wa Syria itamalizwa.

Huu unakua mkutano wa mwisho kwa viongozi wakubwa wawili ambao ni Rais Barack Obama wa Marekani na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambao wanahudhuria vikao hivyo kwa mara ya mwisho wakiwa madarakani.
Rais wa zamani, Lula da Silva kushtakiwa kwa rushwa

Jaji mmoja nchini Brazil amekubali mashataka ya rushwa dhidi ya Rais wa zamani wa nchi hiyo Luiz Ignacio Lula da Silva.
Atashtakiwa kwa madai ya kukubali kupokea zaidi ya dola za Kimarekani milioni moja wakati wa mradi mkubwa uliokuwa ukinuka rushwa katika kampuni ya mafuta ya serikali ya Petrobras.
Fedha hizo zinadaiwa kuhamishwa kupitia ununuzi wa ghorofa iliyokuwav ufukweni mwa bahari.
Hata hivyo, Lula da Silva mara nyingi amekuwa akikana madai hayo na kuyaita ni ya msukumo wa kisiasa.
Akiwa mmoja ya wanasiasa mashuhuri nchini Brazil, anatarajiwa kuwania tena nafasi ya urais katika uchaguzi katika kipindi cha miaka miwili.
Awali Lula da Silva alimchagua Dilma Rousseff, ambaye alivuliwa madaraka mwezi uliopita, kuwa ndiye mrithi wake.
Amnesty International yawagusa polisi wa Nigeria

Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International limetoa ripoti, likilaumu Polisi nchini Nigeria kwa utesaji, ukatili na rushwa.
Ripoti hiyo iliyochapishwa leo inadai kwamba, Kitengo maalumu cha Polisi nchini humo kilichoandaliwa kwa ajili ya kupambana na uhalifu, kimekuwa kikitesa watu waliowaweka kizuizini.
Ripoti hiyo inasema kuwa wanafanya hivyo kwa ajili ya kuwatisha kuweza kukiri kosa na kuwafanya waweze kutoa rushwa.
Kwa mujibu wa Amnesty International, Kitengo hicho cha polisi, kinachojulikana kama kikosi maalum cha kupambana na Uhalifu kinaogopwa sana nchini Nigeria, kutokana na ukatili wake.
Wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu wanasema wamepata ushuhuda kutoka kwa watu waliowahi kushikiliwa juu ya jinsi njia za mateso ya kutisha zilivyotumika, ikiwemo kunyongwa, kuachwa na njaa, kupigwa risasi na vitisho vingine huku wakishikiliwa na polisi wala rushwa.
Ripoti hiyo imeeleza pia kikosi hicho maalum cha polisi kimeandaliwa kwa ajili ya kuwalinda watu badala yake kimekuwa kikiwajengea watu hofu na mazingira ya rushwa.
Amnesty Inertaional pia imesema polisi wamekuwa wakivunja haki za binadamu kwa kuwakamata watu, kuwatesa mpaka ''watakapo kiri'' ama kuwapa rushwa maafisa ili waachiwe.
Huwashikilia watuhumiwa hao katika vizuizi tofauti kikiwemo cha Abuja kinachojulikana kama machinjio, ambacho kwa mujibu wa Shirika la Amnesty International kinawashukiwa 130, ikiwa ni watu wengi, zaidi ya uwezo wa jengo hilo.
Hata hivyo Polisi nchini Nigeria bado hawajaijibu ripoti hiyo.
Serikali yafuta shule 44

WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imezifuta shule za awali, msingi na sekondari nchini ambazo hazijasajiliwa zaidi ya 40 kuanzia Julai mwaka jana.
Awali kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, waligundua kuwepo kwa shule 35 zisizosajiliwa na kuzifuta, jambo lililofanya kutangaza shule zote ambazo hazijasajiliwa kujisalimisha ili kusajiliwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Usajili wa Shule katika wizara hiyo, Khadija Mcheka alisema Mei mwaka huu baada kuzipa miezi miwili shule ambazo hazijasajiliwa kufanya hivyo, walizifungia shule nyingine 12.
Mcheka alisema shule zinaweza kufutwa kwa sababu mbili zikiwamo zilizosajiliwa, lakini zikakiuka vigezo ambazo zikitimiza vigezo zinaweza kuomba upya usajili na kupewa.
“Lakini aina ya pili ni zile ambazo hazijasajiliwa na zinaendeshwa kinyume cha sheria ambazo nazo zikifuata taratibu zikatimiza vigezo zinaweza kupewa usajili,” alifafanua Kaimu Mkurugenzi wa Usajili wa Shule.
Alisema katika kipindi hicho mpaka Agosti mwaka huu baada ya tangazo la kuwataka kusajiliwa shule za awali nne, zile za awali na msingi 105 na sekondari 19, walifika wizarani kwa ajili ya kupata taratibu za usajili ambapo zipo zilizosajiliwa na nyingine kupewa vibali.
Alisema katika usajili, kuna wapo waliokidhi viwango na wengine waliopatiwa maelekezo na kupatiwa vibali vya kutumia majengo yaliyopo huku wengine wakipewa vibali vya kujenga majengo ya shule kabla ya kupata usajili.
Alisema kwa shule walizozifungia, waliwaandikia barua za kuwafungia na kuwataka kuhakikisha wanawatawanya wanafunzi katika shule zilizosajiliwa kwa gharama zao bila kuwaathiri wanafunzi.
Alitaja shule zilizofungiwa kwa kuendesha shughuli zake bila usajili kuwa ni shule za awali na msingi za Must Lead ya mkoa wa Pwani, na za mkoa wa Dar es Salaam ni Brainstorm, Pax, Lassana, Grace, Rose Land, Julius Raymod, St Thomas, Mary Mother of Mercy, Noble Sinkonde, Immaculate Heart of Mary, St Columba, Corner stone, Dancraig, Mwalimu Edward Kalunga, Edson Mwidunda, Gisela, Kingstar, St Columba awali, Bilal Muslim, Thado, Hocet , Elishadai, Lawrance Citizen, Comrade, Dar Elite Preparatory na Golden Hill Academy na Hekima.
Nyingine ni Pwani Islamic, St Kizito na Rwazi Encysloped za Kagera, Dancraig na Qunu za Pwani, Hellen’s ya Njombe, Joseph ya Arusha, Samandito na Maguzu za Geita. Alizitaja shule za Sekondari zilizofungiwa kwa sababu hiyo kuwa ni Hananasif, Elu, Hocet, Safina za Dar es Salaam na Namnyaki ya Iringa.
Aidha, Shule ya Fountain Gate ya jijini Dar es Salaam imefungiwa kwa kuendesha bweni bila kibali.
“Baada ya kutoa tangazo kutokana na kubaini kuwapo shule nyingi zisizosajiliwa, wapo waliojitokeza na nyingine tumezifungia kutokana na kutokidhi viwango vya usajili lakini pia tunaamini wapo waliojificha wakiendelea kutoa huduma,” alisema Mcheka na kuwaagiza wakaguzi katika kanda na wilaya, kufanya ukaguzi na kutoa taarifa kwa zile ambazo hazijafungiwa na ikithibitika hazijasajiliwa, kuzifungia mara moja.
Alisema utaratibu uliopo kwa kuhakikisha shule zote zinasajiliwa kulingana na viwango stahili kwa lengo la kutoa elimu bora ni wakaguzi wa kanda, mikoa na wilaya kwa kushauriana na waratibu wa elimu katika kata, kuhakikisha shule yoyote inayochomoza, wanaifuatilia na kuwapa ushauri wa kufuata taratibu za usajili kwa kukidhi viwango stahili.
Alisema wamekuwa wakigundua kuwapo kwa shule, ambazo hazijasajiliwa kutokana na wakati wa mitihani idadi ya wanafunzi inazidi tofauti na walivyosajiliwa na kubainika kuwa wapo waliokuwa wakisoma katika shule, ambazo hazijasajiliwa wanawapeleka katika shule zilizosajiliwa.
“Kuna wenye shule ambazo hazijasajiliwa wakati wa mitihani wanakuja kuomba wanafunzi kufanya mitihani hivyo kuleta usumbufu wa kuwatawanya kwenye shule zilizosajiliwa na kwenda kuwakagua ili kuweza kusajiliwa,” alifafanua.
Msajili huyo alisema madhara yanayotokana na mwanafunzi kusoma shule ambazo hazijasajiliwa ni pamoja na haitajulikana mtoto anachosoma kwani haitajulikana mitaala wanayotumia kutokana na kukosa usajili, hivyo kushindwa kufanya mitihani. Pia mazingira ya shule na mpangilio wake, haitaendana na matakwa ya serikali ya kutoa elimu bora kwani mmiliki atafanya kile anachotaka.
Mei mwaka huu, wizara hiyo ilizipa miezi miwili hadi Julai 30, mwaka huu kuhakikisha shule zote ambazo hazijasajiliwa zinajisajili kabla ya serikali kuzifunga.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk Leonard Akwilapo alisema ifikapo Julai 30, mwaka huu, mmiliki wa shule itakayobainika kutosajiliwa ikiwemo zitakazokosa vigezo vya kusajiliwa, atapaswa kuhamisha wanafunzi waliopo kwa gharama zake.
Alipoulizwa ni shule ngapi ambazo zinajiendesha bila kusajiliwa, Kaimu Mkurugenzi Mcheka alisema tatizo kubwa lipo kwa shule za awali na msingi.
Waziri Mkuu Apokea Mchango wa Watumishi wa Serikali wa Tetemeko la Ardhi Kagera
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea jumla ya sh. bilioni 1.040 kutoka kwa watumishi na wadau mbalimbali zikiwa ni misaada kwa wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, mwaka huu.
Makabidhiano ya michango hiyo, yamefanyika leo mchana (Jumanne, Septemba 20, 2016) kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi hundi kwa Waziri Mkuu, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi alisema kiasi cha sh. 1,000,030,100 kimekusanywa kutoka kwa watumishi wa idara na Wizara zote za Serikali na kwamba michango zaidi bado inaendelea kukusanywa.
“Tunaamini michango hii itasaidia kuwafuta machozi wenzetu waliopatwa na maafa japokuwa tunajua haitatosha kurudisha kile walichopoteza. Tuna imani itasaidia kupunguza makali ya machungu waliyoyapata,” amesema.
Hata hicyo, Balozi Kijazi amemhakikishia Waziri Mkuu kwamba bado wanaendelea kukusanya michango kutoka kwenye nyingine ambazo zilichelewa kupata taarifa na kwamba wakikamilisha wataiwasilisha mapema iwezekanavyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amepokea michango ya sh. milioni 40 na kati ya hizo, sh. milioni 20 zimetolewa na kampuni ya ujenzi ya CHICO ya China na sh. milioni 20 nyingine zimetoka kwa Umoja wa Wafanyabiashara na Wenye Viwanda wa India waliopo nchini (India Business Forum).
Akiwasilisha mchango wake, Mwakilishi Mkuu wa kampuni ya CHICO hapa nchini, Bw. Guo Zhijian alisema wamesikitishwa na maafa yaliyotokea mkoani Kagera. “Tumefanya miradi mingi mkoani Kagera ikiwemo ujenzi wa barabara za urefu kilometa 300, kwa hiyo mkoa huu tunaujua zaidi. Tunatoa pole kwa wote waliopatwa na maafa hayo,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa umoja wa wafanyabiashara na wenye viwanda kutoka India (IBF), Bw. Gagan Gupta alimweleza Waziri Mkuu kwamba wameshtushwa na tukio hilo na kwamba wametanguliza kiasi hicho ili kisaidie juhudi za Serikali katika kukabiliana na maafa hayo.
“Bado tunaendelea kuwasiliana na wenzetu wengine na tukipata michango zaidi tutaiwasilisha mapema iwezekanavyo,” amesema.
Akitoa shukrani kwa waliotoa michango yote hiyo, Waziri Mkuu amewashukuru kwa misaada hiyo na kuahidi kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa walengwa.
“Tunashukuru sana kwa michango yote. Michango hii ni muhimu na inaonyesha mshikamano wa dhati uliopo. Michango hii inaonyesha kuguswa na mapenzi ya dhati kwa waliopatwa na maafa. Napenda niwahakikishie kuwa Kamati za Maafa za Mkoa, Ofisi ya Waziri Mkuu na kamati za wilaya, ziko pale kuhakikisha walengwa wanafikiwa,” ameongeza.
Waziri Mkuu amesema Serikali inakamilisha tathmini ya maafa hayo na kuahidi kutoa taarifa ya kiasi kilichokusanywa na kiasi kilichotumika. Amewaomba wananchi waliotoa ahadi zao za michango wakamilishe ahadi zao.
“Ninawaomba wale walioahidi kutoa michango wakamilishe ahadi zao na wale walio mbali na benki watumie namba za simu zilizotolewa mahsusi kwa ajili ya kuchangia maafa hayo,” amesisitiza.
Akaunti ya maafa imefunguliwa katika Benki ya CRDB yenye namba 015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztz na namba za simu za mkononi zinazotumika kupokea michango hiyo ni 0768-196-669 (M-Pesa) au 0682-950-009 (Airtel Money) au 0718-069-616 (Tigo Pesa).
Tetemeko hilo lililotokea Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu, lilisababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 kujeruhiwa. Kati yao, watu 253 walifikishwa Hospitali ya Mkoa, 153 walilazwa, 113 walitibiwa na kuruhusiwa na wengine 38 wanaendelea na matibabu ambapo kati yao watu 23 wamefanyiwa upasuaji mkubwa na wanaendelea vizuri.
Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM.
JUMANNE, SEPTEMBA 20, 2016.
Marekani yaitupia lawama Urusi, shambulio la Syria

Marekani imesema ndege za kivita za Urusi zinahusika kushambulia msafara wa misaada nchini Syria siku ya Jumatatu na kusababisdha vifo.
Maafisa wa Marekani wameiambia BBC ndege mbili za kivita za Urusi aina ya SU-24, zilikuwa angani, sambamba na msafara huo wa magari, wakati tukio hilo likitokea.
Hata hivyo Urusi imekana na kusema kuwa ndege hizo hazikuwa zake wala za Syria, na kutupia lawama wapiganaji wa waasi.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema ndege zake zinazojiendesha zenyewe zilikuwa zikifuatilia msafara huo, lakini kamera zao zilijizima kabla ya mashambulizi kuanza.
Shambulio hilo la Jumatatu lilifanyika saa kadhaa baada ya serikali ya Syria kutangaza kumaliza wiki ya kusitisha mapigano.
Subscribe to:
Posts (Atom)